Ni imani yangu kwamba mtakuwa wazima wa afya njema na mpo tayari kabisa kusoma kile nilichowaandalia wiki hii rafiki zangu wapenzi. Nitoe shukrani zangu za dhati kwa wote ambao wamekuwa wakinitumia waraka pepe, sms au hata kunipigia moja kwa moja na kunipongeza, nasema ahsanteni sana!
Rafiki zangu, kabla ya k***lizia mada yetu hii ambayo ilianza tangu wiki iliyopita, napenda kuwapa somo fupi sana kwa wapenzi wanapokuwa wamehitilafiana kidogo katika mapenzi yao.
Wengi hujikuta wakianza kugombana na kutoa maneno makali, kama vile ndiyo mwisho wa uhusiano wao, wanakosea sana; kugombana siyo mwisho wa uhusiano, ndiyo maana wakati wakianza kuomba msamaha kwa wenzi wao huanza kuwakumbusha kuhusu kauli zao.
Ndugu zangu, maneno makali yanauma, ni vigumu kusahaulika moyoni na mbaya zaidi, yanaweza kusababisha kupoteza penzi bila sababu. Chunga sana kauli zako kwa mpenzi wako, hasa mnapokuwa katika tofauti. Unaweza ukatoa kauli ndogo sana, lakini ikaharibu kabisa thamani yako kwa mpenzi wako.
Ulimi ni kiungo kidogo sana, lakini kinaweza kusababisha athari kubwa na kufanya maisha yako ya kimapenzi yaharibike kabisa kutokana na jambo dogo tu, maneno yako. Nimeamua kutoa darasa hili kwenu, kutokana na msomaji mmoja ambaye ameniandikia waraka pepe wiki iliyopita akilalamikia kuhusu tatizo hili.
Sina shaka kwamba, ni darasa fupi sana, lakini lililokupa mwanga na kubadilisha kabisa fikra zako. Baada ya hayo, rafiki zangu tunarudi kwenye mada yetu ambayo inakupa mafundisho juu ya mambo ambayo unatakiwa kufanya ili penzi lako linoge, kwa maneno mengine inakuelewesha mambo ambayo hutakiwi kufanya kama ni kweli unahitaji kudumu na mwenzi wako.
Sasa tuendelee...
USIAMINI NGONO KAMA KISHAWISHI CHA KWANZA!
Wanawake wengi wanaharibiwa na hisia kwamba, wanaume wapo nao kwa ajili ya mapenzi (ngono) tu! Kwamba, silaha ya mwisho katika mapenzi yao ni kukutana faragha! Hili limekuwa la kawaida sana kwa wanawake wengi wa sasa.
Kwa wanaowaza hivi, wanakwenda tofauti kabisa na ukweli halisi ulivyo. Mwanaume hayupo na mwanamke kwasababu ya ngono tu. Si kweli kwamba anahitaji ngono kwako ndiyo akawa na wewe. Kama hivyo ndivyo, ingekuwa rahisi sana kwake kutafuta mahali ambapo anaweza kupata ngono, akaachana na mambo ya ‘kujifunga’ na mwanamke mmoja!
Huu ndiyo ukweli ndugu zangu. Wanaume wanapenda wanawake makini, ambao wapo nao kwa ajili ya maisha zaidi. Wanaowaza mambo ya maisha na siyo ngono tu.
Mbaya zaidi, hawapendi kabisa, uoneshe kwamba unajua kuwa yeye ‘hapindui’ kwako kwa sababu hiyo, jambo ambalo halina ukweli.
Ili uwe mwanamke bora, mwenye upeo, huku akiangalia maisha ya baadaye, lazima uwe mnyenyekevu kwa mpenzi wako, mshauri wake mkuu na uwe naye karibu sana hasa anapokuwa kwenye matatizo.
Wakati mwingine kumpigia simu tu, wakati anapokuwa mgonjwa au mwenye msongo wa mawazo, kunaweza kukuongezea pointi za mke bora hapo baadaye, na wala si ngono kama baadhi ya mawazo ya hovyo ya baadhi ya watu. Ondoa uchafu huu akilini mwako, ngono si kila kitu kwenye mapenzi rafiki zangu.
KUTOTAFUTA SULUHU KATIKA UHUSIANO
Mwerevu ni yule anayegundua kwamba amekosea halafu anaanza upya kutafuta njia za kutoka kwenye makosa. Huu ndiyo werevu. Siku zote mwanamke mwenye busara na nia njema na uhusiano wake, hapendi kumkosea mpenzi wake na hata kama akifanya hivyo, anakuwa mwepesi sana wa kutafuta njia za kuweka sawa uhusiano wake.
Kama unakosea, unatambua, halafu unakaa kimya, utasomeka kama una kiburi. Siku zote wania kuwa mwerevu katika uhusiano wako na kuhakikisha kwamba, mwenzi wako anakuwa na furaha kama siyo kufurahia penzi lenu.
“Sweetie, sikujua kama jana ungekasirika, hata nilipokuwa nafanya vile, akilini mwangu sikuwaza kama ungechukia. Nimekosea baby, naomba unisamehe,” ujumbe mfupi wa maneno kama haya ukiutuma kwa mwenzi wako asubuhi ya siku ambayo ulikuwa naye kwenye mtoko na kumuudhi, itaweza kudumisha uhusiano wenu.
EREVUKA...
Mapenzi ni kujifunza na pia unatakiwa kufahamu kwamba hakuna mbabe wala mjinga wa mapenzi. Ukijua kosa lako, utajirekebisha na kuboresha uhusiano wako, wakati ukitafuta elimu zaidi juu ya mapenzi.
Ulilofanya jana ukagundua leo kwamba ulikosea, ni wazi kwamba huwezi kulirudia tena maana tayari utakuwa umeshapata ukweli wa ulichokosea. Ukijifunza leo kitu kipya, kesho na keshokutwa, mtondogoo unaweza kuwa bora zaidi katika uhusiano wako maana tayari utakuwa umeshaerevuka.
Makosa haya usikubali kuyafanya tena, badilika huku ukiendelea kujifunza zaidi. Kumbuka kuna mengi ambayo hufanywa kimakosa na wanawake bila kujua, lakini haya ni yale ya muhimu zaidi.
No comments:
Post a Comment