HAKUNA msanii wa kike wa Bongo anayemuweza Jaydee. Ndivyo walivyosema mashabiki walioshuhudia mambo yake kwenye shoo ya kutimiza miaka kumi iliyofanyika Dar es Salaam Ijumaa usiku.
Msanii huyo alifunika kuanzia mavazi, sauti na nyimbo zake na aliuthibitishia umma uliofurika kumuona kwa vitendo kwamba yeye ni wa levo nyingine.
Shoo hiyo iliyofana ilifanyika kwenye Ukumbi wa Millenium Tower, Kijitonyama jijini Dar es Salaam ilikuwa mshikemshike kwa jinsi mashabiki walivyohaha kusaka tiketi kuingia ndani kwa vile umati ulikuwa mkubwa sana.
Msanii huyo sambamba na bendi yake ya 'Machozi' walionyesha umahiri mkubwa katika kupangilia vyombo hali iliyoongeza hamasa kwa washabiki ambao hawakuamini kama Jaydee yuleyule wa muziki wa kizazi kipya ndiyo anang'ara na bendi.
Mashabiki walianza kupagawa wakati alipoanza kuimba nyimbo za zamani zilizobamba watu enzi hizo, kama 'Mawazo', 'Wanaume Kama Mabinti' na nyinginezo ambazo watu walikuwa wakimsapoti kwa kuimba naye.
Chegge wa Kundi la Wanaume Family alipanda jukwaa na kuimba na msanii huyo ndipo kelele ziliporindima zaidi ukumbini hapo maarufu kama Mzalendo Pub. Jaydee aliimba wimbo wa 'Mambo Bado' pamoja na Chegge lakini walipomaliza katu mashabiki hawakutaka Chegge ashuke ikaahidiwa kwamba atarudi baadaye.
Wasanii wengine waliomsapoti Jaydee ni Keisha, TID na wimbo wa 'Distance' alioshirikishwa mwaka 2004 kwenye albamu ya 'Moto'
Pamoja na yote hayo Jay Dee alizindua albamu mpya yenye nyimbo 12 iitwayo 'Combination' aliyoimba na Machozi Band.
Miongoni mwa nyimbo zilizomo ndani ya albamu hiyo ni 'Raha', 'Siku ya Kufurahi',' Teja' , 'Elimu Shule', 'Tunakuja', 'Nilivyo' na 'Uko Juu'.
Nyingine ni 'Nilizama', 'Inuka Simama' na 'Natamani Kuwa Malaika', ambapo baadhi zimeshasikika mtaani.
Pamoja na shoo nzuri kutoka kwa Jay Dee na bendi yake mashabiki walilalamikia udogo wa ukumbi hali ilifanya watu kushindwa kujiachia inavyotakiwa.
Msanii huyo aliimba kwa muda mrefu na kuonyesha manjonjo ya kila aina bila kuchoka na kuuthibitishia umma kuwa ana kipaji na anaangalia mbele kwa mbele kuzidi kutoa kazi nzuri zaidi kuzidi kudhihirisha ubora wake unaomtofautisha na wasanii wengine wa kike nchini, ambao wamekuwa wakiibuka na kupotea. Mbali na shoo kulikuwa na kulishwa keki maalumu kwa watu mbalimbali waliomuwezesha kufikia mafanikio yake.
No comments:
Post a Comment