Ni wiki nyingine tunakutana tena kupitia safu hii namba moja kwa kuandika makala kali za kimapenzi nikiamini kwamba umzima wa afya na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida. Mimi namshukuru Mungu kwa mema yote ambayo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu.
Mpenzi msomaji wangu, nina imani kila mmoja anayesoma makala haya ana imani yake nikimaanisha kwamba, kama wewe siyo Muislamu basi utakuwa ni Mkristo. Kwa Waislam kote ulimwenguni kipindi hiki wanaingia katika kutimiza moja ya nguzo kuu ya dini yao, kufunga. Hili kuna wapenzi ambao linawagusa moja kwa moja nikiwa na maana ya kwamba, kuna wale ambao ni wapenzi na wote ni Waislamu lakini pia yawezekana wewe ni Mkristo na mpenzi wako akawa ni Muislamu.
Sasa basi, ikiwa wewe una mpenzi wako ambaye ni Muislamu na wewe pia ukawa ni Muislamu natumaini mtakuwa mnatambua namna ambavyo mnatakiwa kuishi katika kipindi hiki. Yapo mambo ambayo huko nyuma mlikuwa mkiyafanya lakini kwasasa mtalazimika kuyaweka pembeni kama siyo kuyaacha kabisa. Lakini pia huenda wewe ni Mkristo na una mpenzi wako ambaye ni Muislamu, itakuwa ni busara sana kama utaonesha kumpenda kwa kumuacha atimize imani yake hiyo kwa uhuru bila kubughudhiwa.
Yawezekana wapo ambao wanajiuliza sababu hasa ya mimi kuamua kuandika makala haya. Juzi nilipata kesi kutoka kwa mmoja wa wasomaji wangu akieleza kuwa, ameachwa baada ya kumweleza mpenzi wake kuwa, kwa kipindi hiki uhusiano wao utakuwa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
“Mpenzi wangu ni mkristo na mimi ni muislam, katika uhusiano wetu tulizoea kukutana mara kwa mara faragha kama ilivyo kwa wapenzi. Zaidi ya yote, kuna mavazi ambayo nimekuwa nikiyavaa, kwakweli hayaendani na mafundisho ya dini yetu ila yeye amekuwa akifurahi sana akiniona nimeyavaa na amekuwa akiniambia maneno kama vile; “Umependeza sana mpenzi wangu.”
Ila mimi kama Muislamu nina wajibu wa kufunga na kujaribu kujiepusha na yale ambayo yanaweza kuiharibu funga yangu kama vile kuwa mbali na mpenzi wangu ambaye hajanioa, kuvaa mavazi ya heshima na mambo mengine kama hayo. Cha kushangaza nilipojaribu kumshirikisha mpenzi wangu katika hili, hakukubaliana na mimi. Nampenda sana mpenzi wangu huyu lakini nashindwa kujua kwanini anashindwa kuiheshimu imani yangu,”anaeleza Farida wa Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Aliyoniambia Farida ndiyo yaliyonisukuma kuandika makala haya nikiamini yatawagusa walio wengi popote walipo. Ninachotaka kukisema hapa ni kwamba, kama tunavyojua kwamba mapenzi hayachagui dini.
Na ndiyo maana tunashuhudia kila siku msichana Muislamu akionesha kumzimikia kijana wa Kikristo na kinyume chake pia. Hivyo, nina uhakika kabisa kwamba kuna wapenzi wengi walio katika mazingira hayo huku wengine wakiishi kama mke na mume lakini wakiwa katika imani tofauti. Inapotokea hivyo, kuna kila sababu ya kila mmoja kuiheshimu imani ya mwenzake.
Wewe ni Mkristo na mpenzi wako ni Muislamu,msaidie katika kumfanya atimize yale anayopaswa kuyafanya kwa mujibu wa dini yake. Kamwe usiwe msitari wa mbele kumuwekea vipingamizi visivyo na msingi.
Muwekee mazingira mazuri ya kutimiza ibada hii. Kaeni mbali katika suala la kukutana faragha,mkubalie avae mavazi ya kujistiri na pia unatakiwa kumuepusha na vishawishi. Kwa mfano wewe ni msichana na una mpenzi wako Muislamu, masuala ya kumvalia nguo za kimitego hayana nafasi katika kipindi hiki kwani unaweza kumtamanisha na mwisho akajikuta anashinda na njaa tu badala ya kufunga.
Hapo ndipo yataonekana mapenzi ya kweli. Aidha, hiki kisiwe ndiyo kipindi cha kusalitiana. Kama nilivyosema hapo awali kwamba, wengi wapo katika uhusiano na watu wa dini nyingine sasa basi, kama dini haiwaruhusu kukutana faragha, kuwa na moyo wa subira,endelea kumpenda, kumheshimu na kumjali mpenzi wako pale inapobidi.
Kwa wale ambao wamebahatika kuwa wapenzi na wote ni Waislamu, wao watakuwa wanajua yapi ya kufanyiana na yapi ya kuyaepuka na mwisho wakapata kile walichokitarajia kutoka kwa Mungu wao.
Kikubwa nisisitize kuheshimu imani za wenzetu, tuwaepushe na vishawishi ambavyo vinaweza kuwatia katika majaribu na mwisho kuambulia sifuri. Wale ambao watakasirika na kufanya usaliti eti kwasababu wapenzi wao wamebadilika kwa ajili swaumu, hao watakuwa ni wababaishaji na kwa jina lingine tunaweza kuwaita matapeli wa mapenzi.
Jamani ni hayo tu kwa leo, niwatakie Waislamu wote funga njema na naomba niseme hivi, kama nyie ni wapenzi tu na wote ni Waislamu, mnapofunga muombeni Mungu mwezi mtukufu ujao uwakute mkiwa ndani ya ndoa. Kama wewe mpenzi wako ni Mkristo, pia muombe Mungu awabadili aidha wewe kubadili dini ama mpenzi wako kukufuata wewe kisha mfunge ndoa na kuyafurahia maisha yenu. Pia kama nyie ni wanandoa wakati mnafunga muombeni Mungu awajaalie ndoa yenu idumu na awaepushe na mahasidi ambao wamekuwa wakikosa amani wanapowaona watu wanapendana.
No comments:
Post a Comment